Habari

Jack Ma Arudi Uraiani Baada ya Kimya cha Miezi Miwili

Ma alipotea machoni mwa umma tangu Octoba mwaka jana baada ya kuwakasirisha wadhibiti katika hotuba yake ya Oktoba 24 wakati wa kongamano mjini Shanghai

Baada ya kimya cha miezi miwili na nusu, mfanyabiashara mashuhuri nchini China, Jack Ma leo alionekana akihutubia baraza la walimu huku uchunguzi wa biashara zake ukiendelea.


Bilionea huyo alionekana katika video ya sekundi 50 akiwapongeza walimu wanaofadhiliwa na wakfu wake na hakutaja hatua ya kupotea kwake machoni pa umma ama juhudi rasmi za kuimarisha udhibiti wa kampuni ya Alibaba na kampuni nyingine za intaneti katika muda wa miezi sita.

Jack Ma pia alishawahi kuwa mwalimu wa Kiingereza kabla ya kugeukia ujasiriamali na kujenga kampuni kubwa ya biashara mtandaoni ijulikanayo kama Alibaba.

Habari hiyo ilioneshwa kwa mara ya kwanza na tovuti ya Habari ya Tianmu iliyoko Zhejiang mashariki mwa China.

Ma alipotea machoni mwa umma tangu Octoba mwaka jana baada ya kuwakasirisha wadhibiti katika hotuba yake ya Oktoba 24 wakati wa Kongamano mjini Shanghai. Siku chache baadaye, wadhibiti hao walisitisha mipango iliyokuwa imepangwa kufungua soko la hisa la mabilioni ya dola ya kundi la Ant, ambalo ni jukwaa la kifedha lililoibuka kutokana na huduma ya malipo ya Alibaba inayojulikana kama Alipay.