Habari

IGP Sirro; Tunapeleleza kuhusu QNET tutawapa wananchi ukweli wa mambo

Baada ya muda mfupi tutapata majibu na tutawaambia wananchi ukweli

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Simon Sirro amesema Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha upelelezi kimeunda kikosi maalumu kwa ajili ya kufanya upelelezi ili kubaini ukweli kuhusu tuhuma za utapeli dhidi ya makampuni mbalimbali ikiwemo tuhuma za hivi karibuni dhidi ya kampuni ya QNET. IGP Sirro ameyasema hayo Disemba 19, 2020 wakati akijibu maswali ya wanahabari mkoani Geita ambapo amekuwa kwa ziara ya kikazi. 

 

“Kauli yetu [Jeshi la Polisi] ni uchunguzi, tumepata [taarifa] kuhusu haya makampuni yananayotuhumiwa kwa utapeli, tumefungua jalada la uchunguzi na nimemwelekeza Mkurugenzi wa Upelelezi ameunda kikosi maalumu kupeleleza ili kupata ukweli. Baada ya muda mfupi tutapata majibu na tutawaambia wananchi ukweli.” – amesema IGP Sirro 

 

Akizungumzia kuhusu suala la ulinzi na usalama mitandaoni, IGP Sirro amesema Jeshi la Polisi limejipanga kushughulikia uhalifu wa kimtandao kuanzia ngazi ya wilaya ili kuhakikisha upelelezi unafanyika kwa ufanisi na hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wahalifu. Kamanda Sirro ameongeza kwamba katika kuhakikisha usalama mtandaoni, jeshi la polisi limeendelea kuwapa mafunzo ya mara kwa mara maafisa wake ili kuweza kukabiliana na dhana hiyo ngeni ya uhalifu. 

 

“Sasa hivi makosa mengi yanafanywa kwa njia ya mtandao, tulichofanya ni kuhakikisha kwamba upelelezi wa makosa ya kimtandao unafanyika kuanzia ngazi ya Wilaya tofauti na mwanzo ambapo uchunguzi ulifanyika katika ngazi ya Mkoa na ofisi ya Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi pekee. Lakini pia tumetoa mafunzo mengi sana kwa  askari wetu na kuhakikisha kila wilaya kuna kiongozi anayesimamia upelelezi wa makosa ya mtandao.” – amenukuliwa IGP Sirro.