Habari

Hayati Jerry Rawlings, Rubani wa Ndege za Kivita aliyeitawala Ghana kwa miaka 20

Aliongoza mapinduzi mawili ya kijeshi kabla ya kuongoza nchi yake kuelekea utawala wa kidemokrasia.

Jerry John Rawlings aliyekuwa Afisa wa Jeshi na mwanasiasa nchini Ghana, aliongoza mapinduzi mawili ya kijeshi kabla ya kuongoza nchi yake kuelekea utawala wa Kidemokrasia. Ameaga dunia Jumanne ya Novemba 12, 2020 akiwa na miaka umri wa 73.

Jerry alizaliwa mwaka 1947, na mauti yake  yamemkuta akiwa katika hospitali ya Korle Bu huko katika jiji la Accra nchini Ghana akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Rais Nana Akufo-Addo amesema “mti mkubwa umeanguka, Taifa la Ghana limepoteza kitu cha thamani sana”. Rais Nana ametoa pole kwa familia ya marehemu na kutangaza bendera zote kupepea nusu mlingoti kwa siku saba huku nchi hiyo ikijiandaa na shughuli za msiba huo.

Hayati Rawlings alizaliwa na baba Mskochi huku mama yake akiwa Mghana ambaye naye alifariki mwaka huu akiwa na umri wa miaka 101. Rawlings alikuwa ni mwanajeshi aliyebobea kwenye masuala ya anga akiwa ni rubani mahiri katika kurusha ndege za kivita ambapo mwaka 1969 alitukunukiwa tuzo ya “Speed Bird Trophy” baada ya kufanikiwa kurusha ndege ya kivita aina ya Su-7.

Mwaka 1978 alikabidhiwa cheo cha Uluteni katika Jeshi la Anga la Ghana, ilipofika mwaka 1979 Hayati Rawlings akiwa na wanajeshi wengine sita waliongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya utawala wa kijeshi wa Jenerali Fred Akuffo ambaye aliingia madarakani mwaka 1978, mapinduzi hayo hayakufanikiwa hali iliyopelekea yeye pamoja na wenzake kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwenye mahakama ya kijeshi ambako alihukumiwa adhabu ya kifo. Lakini kauli zake za kishujaa kuhusu hali ngumu ya maisha kabla ya kukamatwa zilimpatia wafuasi wengi.

Juni 4, 1979 akiwa anasubiri siku ya hukumu yake ya kifo kufika alikombolewa gerezani na kundi la wanajeshi waliovamia gereza alikofungwa. Akiwa ameshikilia ajenda ya rushwa iliyokithiri kwenye serikali ya Jenerali Fred Akuffo na kwamba serikali mpya inahitajika ili kuleta mageuzi na maendeleo ya kweli, aliongoza kikundi cha wanajeshi ambao walimpindua Jenerali Akuffo na uongozi wake.

Baada ya mapinduzi hayo aliunda kundi lenye wajumbe 15 lililoitwa Armed Forces Revolutionary Council (AFRC), na walitawala kwa siku 112 wakapanga mauaji ya halaiki ya wanajeshi 8 wenye vyeo vya juu watatu kati yao walishakuwa wakuu wa nchi hiyo, Afrifa, Acheampong, na Akuffo.

Septemba 24, 1979 alikabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia wa Rais Hilla Limann kutoka chama cha PNP ambacho kilikuwa kinaungwa mkono na wafuasi wa Rais wa kwanza wa Taifa hilo Kwame Nkurumah. Miaka miwili baadaye, Desemba 31, 1981 Rawlings aliongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Hilla Limann akidai utawala wa Rais huyo ulikuwa dhaifu na uchumi wa nchi hiyo ulikuwa kwenye hali mbaya.

Rawlings alianzisha chama chake kilichoitwa PNDC ambacho kilileta sera mbalimbali za mageuzi ya kiuchumi ambayo hazikuwa na mafanikio sana. Kufikia mwaka 1983 Taifa hilo lilikumbwa na mgogoro wa kiuchumi ambao mabadiliko ya kimfumo hali iliyomlazimu kuitisha uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na ukafanyika mwaka 1992.

Katika utawala wake alianzisha mchakato wa Katiba mpya na kufanikiwa kuandika Katiba mpya ya Kidemokrasia iliyoruhusu vyama vingi na uundwaji wa Tume huru ya uchaguzi. Katiba hiyo iliweka ukomo wa Urais kwa kuweka vipindi viwili vya Urais vya miaka mitano.

Kwa mujibu wa Katiba hiyo mpya ya utawala wa kiraia kipindi chake cha uongozi kilifikia mwisho mwaka 2001 ambapo alistaafu na nafasi yake kuchukuliwa na John Agyekum Kufuor mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi wa 1996.

Baada ya kustaafu aliteuliwa kwenye kazi kadhaa za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ikiwemo Mjumbe maalumu wa AU kwa nchi ya Somalia.

Jerry Rawlings atakumbukwa kama Rais aliyeweka misingi ya kidemokrasia katika Taifa la Ghana kwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi na mchango wake katika kuleta Katiba mpya ya kwanza ya vyama vingi ambapo kwa sasa Ghana inatajwa kama moja ya nchi kwenye Ukanda wa Afrika ya Magharibi ambayo Demokarasia yake imekomaa.

Akiwa Rais pia atakumbukwa kwa kuhimiza uwekezaji kwenye sekta za mafuta na dhahabu. Pia atakumbukwa kwa kuikuza taswira ya Ghana Kimataifa kwa kupeleka wanajeshi wake kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa kwenye kulinda Amani kwenye nchi za Liberia, Sierra Leone, Lebanon na Iraq.

Hayati Jerry John Rawlings ameacha mjane, Nana Konadu Agyeman, watoto wa kike watatu,  Zanetor Rawlings, Yaa Asantewaa Rawlings, Amina Rawlings; na wakiume mmoja, Kimathi Rawlings.