Burudani

Harmonize, Rayvanny wanavyotembelea kiki

Wasanii wengi wa Bongo Fleva na filamu wamekuwa wajanja wa kucheza na hisia za mashabiki ambao wanaonekana kulevywa na mapenzi

Ndiyo! Ni kiki, wala haihitaji kutazama mara mbili mbili. Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wapendanao kila mmoja kwa nafasi yake alifanya mbwembwe zake ilimradi kumfurahisha yule mwenye ukaribu zaidi na moyo wake. Tunaweza kusema michoro na emoji za kopa viliteseka sana siku ya jana kwani zilitumiwa hata kwa watu wasio na nia njema na mapendo.

 

Kila mtu alitumia ubunifu na kipaji kwa kadiri alivyojaliwa kuwasilisha hisia zake za huba. Kwa wale tusio na vipaji ilitosha kutumia ujumbe mkuu wa ‘Happy Valentine’ au Heri ya Valentine na kwa vile wapendwa wetu wametukubali bila kuwa na vipaji, walikubaliana na hali. Hata kama wasingekubali ingewapasa kusubiri hadi msimu mwingine kwani ubunifu hauji kwa bahati mbaya.

 

Katika masuala ya mapenzi utakubaliana nami kwamba kila mtu ana kasi yake lakini hata kasi ya Usain Bolt haijazidi kasi ya wasanii. Wasanii wamekuwa mstari wa mbele kuonesha hisia zao bila kujali aina ya hisia. Na kwa hapa nyumbani Tanzania wasanii wetu wanasema ‘HipHop Hailipi’ kwa maana kwamba muziki au kazi ya sanaa inayowasilisha ujumbe usiobeba dhima ya mapenzi utapata wafuasi wachache na kujikuta muwasilishaji/msanii hapati maslahi mapana kama wanayopata wahubiri wa mapenzi.

 

Wasanii wengi wa Bongo Fleva na filamu wamekuwa wajanja wa kucheza na hisia za mashabiki ambao wanaonekana kulevywa na mapenzi. Wasanii wamekuwa wakitunga maelfu ya nyimbo kuizunguka dhima hiyo na kama haitoshi wamekuwa wakitumia mahusiano ya mapenzi kama namna ya kuvuta attention ya mashabiki. Wenyewe wanaita kiki.

 

Wasanii wengi wa-kike kwa wa-kiume wamekuwa wakitumia mahusiano yao au hata kutengeneza mahusiano feki kwa lengo la kuvuta umma kufuatilia kazi zao na kuwafanya waendelee kubaki juu katika kazi yao ya sanaa. Mbinu hii ambayo haiungwi mkono na baadhi ya waumini wa burudani imekuwa ikitumika sio tuu kwa wasanii wa Tanzania bali kila pembe ya dunia.

 

Sijui labda mapenzi ndio kitu chenye mguso na nguvu zaidi kwa binadamu na ndio maana wengi hupenda kupata uzoefu wa watu wa maarufu kwenye mahusiano. Suala la mapenzi kuwa na mguso na nguvu zaidi kuliko kitu chochote laweza kuwa la mjadala wa kidunia. Wengi tunajua jinsi penzi la Beyonce na Jay Z linavyowafanya kufuatiliwa sana duniani.

 

Nani asiyekumbuka penzi la Complex na Vivi au penzi la komando Lady Jay Dee na Gadner? Penzi la Vanessa na Jux? Au basi penzi lililosumbua la Diamond na Wema?

 

Lakini hapa tumulike namna ambavyo kwa mwezi huu unaoitwa na baadhi ya washadadia mapenzi ‘mwezi wa wapendanao’ tumefanywa kusahau uwepo wa UKOVI-19 – ugonjwa hatari unaokatisha maisha ya wengi kote duniani. Katika muziki tukiachana na nyimbo na albamu kali zilizoachiwa mwezi huu. Masuala ya ‘Valentine’ yametikisa sana ambapo Harmonize pamoja na Rayvanny wameendeleza mbinu ya kutumia kiki ya mapenzi kuwafanya kuzungumziwa zaidi Tanzania bara na visiwani.

 

Alianza Harmonize kwa kuimba kipande cha wimbo uliomlenga mwanamke asiyejulikana. Kipande hicho cha wimbo kinachojulikana kama ‘Mtaje’ akiwa anataja sifa za mwanamke anayetamani kuwa naye katika mahusiano na kuwaachia kazi mashabiki wake kutumia sifa hizo kumtambua mwanamke huyo. Harmonize alionekana kulalama kwamba nyota yake haikukubalika kwa Kajala enzi hizo akiwa rafiki na Wema Sepetu ila bado yeye anampenda mbali na kwamba amemzidi umri.

 

“…Hivi niseme ana ngekewa, ama nyota yake kali amenizidi,

Ama mjini nimechelewa, mbona wengine wanamponda wanamwita bibi…,”

 

Hayo ni sehemu ya mashairi ya Harmonize akilalama kwenye Mtaje.

 

Mashabiki wenye ufikiri wa haraka tayari walishamtaja Kajala Masanja hata kabla ya kipande hicho hakijamalizika. Wakati mashabiki wakiendelea kufurahia uzuri wa kipande hicho, ghafla picha za wawili hao wakiwa katika dimbwi la mapenzi zikaibuka. Mjadala kuhusu tofauti ya umri wa Kajala na Harmonize sio jambo la kujadili kwani lilishapitwa na wakati – kikubwa wawili hao wanafurahia ufuasi mkubwa na kuendelea kujihakikishi nafasi za ubalozi wa chapa mbalimbali ambazo huko ndiko wasanii hupata pesa za kuendelea kulipa kodi.

 

Kajala (kushoto) akiwa na binti yake Paula kwenye moja ya kazi za ubalozi wa chapa ya taulo za kike


Rayvanny ambaye ameachia albamu kali ya ‘Sound from Africa’ angeweza kuendelea kusumbua kwa mwezi mzima bila kujihusisha na familia ya Kajala. Lakini akaona isiwe kesi, kwa nini kiki apate Harmonize peke yake wakati anaweza kulipia gharama za kiki?

 

Wakati watu wakiwa bize kujenga na kuhuisha mapenzi yao katika siku ya wapendanao, Rayvanny naye akaja na mtindo wa kiki aliotumia Harmonize yeye akiimba kipande cha wimbo unaokwenda kwa jina la ‘Valentine’. Katika wimbo huo Rayvanny anakiri kumfungulia moyo binti wa Kajala aitwaye Paula – binti anayesumbua katika mtandao wa Instagram kwa kile wataalamu wa urembo wanachokiita uzuri wa sura na umbo.

 

Sehemu ya mashairi ya Valentine wa Rayvanny yaliyoandikwa kwa ustadi ni inaeleza binti huyu sio mkubwa kiumri ingawa ni mrembo na aliyeumbika vizuri. 

 

“…Moyo wake wa thamani amenipa bure, mtoto shepu kaitupa kule,

Sio wa zamani 2000 mule mule, kadogo kadogo utasema kapo shule,…”

 

Rayvanny anaendelea kueleza kwamba yuko tayari kutoa mahari kwa famila ya Paula ambaye kwa mujibu wake anasema ana chembechembe za uzuungu na usukuma.

 

“…Ana uzungu chembechembe za Mwanza

Nitatoa mali kwa mzee Massanja”

 

Hii ya Rayvanny imesambaa haraka kwani mbali na kuimba dedikesheni hiyo ya Siku ya Wapendanao na kukiri kutaka kupeleka mahari kwa mzee Massanja (babu wa Paula) tayari kuna video zinazowaonesha wawili hao wakifurahia mahusiano. Mazungumzo mengi yameibuka katika mitandao kuhusu video hizo na mahusiano hayo jambo lilifanya Kajala kumpa likizo Harmonize na kuanza kushughulikia suala la binti yake.

 

Kwa kutazama mtiririko huu wa matukio ni rahisi kusema kwamba mbinu ya kutengeneza au kutumia mahusiano ya kimapenzi kwa lengo la kuvuta mashabiki ni mbinu inoyokosolewa lakini yenye mafanikio kwa wengi. Wasanii wengi wanaofuatiliwa zaidi ni wale wenye uwezo wa kutengeneza kiki.

 

Kuna wale watakaouliza mbona hujamzungumzia Kala Jeremiah na picha zake za harusi kumbe anakuja na wimbo wa Wewe? Hahaah! Akili za kuambiwa changanya na zako.