Afya

Fahamu Umuhimu wa Kufanya Vipimo Vya Afya Mara kwa Mara

Dalili za magonjwa mengi yasiyoambukiza huchukua muda mrefu kuonekana, yaani muda kati ya mtu anapopata ugonjwa na muda wa dalili kuanza kuonekanahuwa ni mrefu ukilinganisha na magonjwa yanayoambukiza.

 

Tafiti zinanonesha kuwa 71% ya vifo vyote duniani husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza. Kwa hivyo, magonjwa haya yasiyoambukiza yamechukua sehemu kubwa ya sababu za vifo zinazotokana na magonjwa.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna magonjwa makuu manne yasiyoambukiza; magonjwa ya moyo, saratani, magonjwa ya mfumo wa upumuaji na kisukari.

 

Magonjwa haya manne yanahusishwa zaidi na aina nne za tabia maisha yaani, uvutaji wa sigara, matumizi ya vilevi/pombe, kutokujishughulisha, na ulaji mbaya.

 

Tabia maisha hizo nne zinapelekea mabadiliko ya mwili ambayo husababisha kuongezeka kwa shinikizo la damu, uzito kupita kiasi, kuongezeka kwa mafuta kwenye damu, na kuongezeka kwa kiwango cha sukari kwenye damu.

 

Leo tujadili zaidi kuhusu kuongezeka kwa kiwango cha sukari kwenye damu, badiliko mwili linalosababisha ugonjwa wa kisukari kama isiporatibiwa.

 

Mgonjwa mmoja alikuja maabara kwaajili ya kupima kiwango cha sukari kwenye damu, ni mwanaume mwenye miaka 53. Alipima sukari bila kula kwa masaa nane (fasting blood sugar).

 

Majibu yalikua ni 16.2mmol/L, ikimaanisha kuwa kiwango cha sukari kwenye damu ni kikubwa kuliko kawaida, kwa kawaida inatakiwa iwe kuanzia 4.0 hadi 7.0mmol/L.

 

Kabla ya kumpa majibu yake nilimuuliza kama alishawahi kufanya kipimo cha sukari. Akanijibu hakuwahi kupima kabisa na ndiyo mara yake ya kwanza.

 

Akanitaarifu kuwa hupata uchovu mara kwa mara, haja ndogo mara kwa mara, anapata kiu ya maji mara kwa mara, pamoja na kuona makengeza wakati fulani ambazo ni baadhi ya dalili za ugonjwa wa kisukari.

 

Nilimshauri aende kwa daktari ili amsaidie ushauri na namna ya kupanga matibabu.

 

Daktari alitaka nimfanyie kipimo cha aina ya chembe damu inayohusika kuratibu sukari kwenye damu kwa miezi mitatu (HBA1C). Kipimo hiki ni muhimu sana kwani kinatoa kielelezo vizuri namna gani mwili unavyoratibu kiwango cha sukari kwenye damu.

 

Majibu ya kipimo hiki yalikuwa 12.6% ambayo ni kubwa kuliko kawaida, kwa kawaida hupaswa kuwa (0.1-6.5%). Kwa majibu ya kipimo hiki inamaanisha kuwa ana kisukari.

 

Kutoka kwa mgonjwa huyu tunatumaini utakuwa umejifunza kitu, kama angekuwa na utaratibu wa kupima kiwango cha sukari mara kwa mara basi angeweza kuiratibu mapema kabla haijafika kiwango kikubwa sana.

 

Hakufanya hivyo kwasababu hakuona dalili yeyote ya kisukari, baada ya kuona dalili za kisukari ndipo alipokuja hospitali kupima. Tufahamu kuwa dalili za kisukari huchukua muda mrefu sana kuanza kuonekana, kwahiyo unaweza kuwa na tatizo lakini dalili bado hazijaanza kuonekana.

 

Ni vizuri tuwe na desturi ya kufanya vipimo vya afya mara kwa mara hata kama hatuoni dalili yeyote ya ugonjwa na suala hili liwe ni utaratibu endelevu katika maisha yetu, hii itasaidia zaidi kutambua tatizo mapema na kurahisisha mipango ya matibabu pia kupunguza kiwango cha magonjwa yasiyoambukiza.

 

Na Gospel Haule,

Mtaalamu wa Maabara za Afya