Afrika

#ENDSARS: Serikali ya Nigeria Imetangaza Kukifuta Kitengo Maalumu cha Kukabiliana na Ujambazi, SARS.

Hatua hiyo inafuatia maadamano makubwa ya vijana yaliyoibuka nchini humo kutaka kufutiliwa mbali kitengo hicho kutokana na tuhuma za ukatili kwa raia

Serikali ya Nigeria imekifuta kitengo cha Polisi cha kukabiliana na Ujambazi (SARS) baada ya siku kadhaa za maandamano yaliyopinga ukatili wa polisi. Kwa muda mrefu Special Anti-Robbery Squad (SARS) wamekuwa wakituhumiwa kwa udhalilishaji, ukamataji haramu, utekaji, utesaji na mauaji ya raia wasiokuwa na hatia.


Mkuu wa Jeshi la Polisi amesema kuwa kuanzia sasa kitengo hicho kimefutwa na polisi waliokuwa wanahudumu watahamishiwa kwenye vitengo vingine ndani ya jeshi hilo.


Wasanii Davido, Wizkid, Falz, Tiwa Savage, Burna Boy na Runtown ni miongoni mwa majina makubwa waliounga mkono maandamano ya #ENDSARS yaliyotaka kufutwa kwa kitengo hicho cha Polisi
huku wanaharakati ndani ya Nigeria na sehemu nyingine duniani wakitumia #ENDSARS mitandaoni kushinikiza mageuzi kwenye jeshi la Polisi.

 

Kwa miaka kadhaa iliyopita, video na picha mbalimbali zimekuwa zikisambazwa mitandaoni zikiwaonesha watu wanaotuhumiwa kuwa maofisa wa polisi wa kitengo hicho wakipiga raia, kuwadhalilisha, kuwataka watoe rushwa na wakati mwingine kuua watuhumiwa ambao hawakukataa kuwa chini ya Ulinzi.

 

Tovuti imeanzishwa yenye kikoa https://endsars.com/ ambayo inawataka raia ambao walishakutana na ukatili wa kitengo hicho kuelezea masahibu yao, ambapo mamia ya watu tayari wameshachapisha kuelezea makadhia yaliyowakumba walipotiwa nguvuni na kitengo hicho, huku wengine wakielezea masahibu yaliyokwakuta ndugu zao wa karibu yakiwamo mauaji bila uthibitisho wa uhusika wa wahanga kwenye uhalifu.

 

Mwaka 2018 baada ya malalamiko makubwa kuhusu utendaji kazi wa kitengo hicho, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari aliahidi kuleta mageuzi katika kitengo hicho, ingawa miaka miwili baadaye hakukuwa na mabadiliko ya wazi ambayo raia wa taifa hilo waliridhika nayo.

 

Katika taarifa yake, Mkuu wa Jeshi la Polisi amesema kuwa kitengo hicho kimefutwa mara moja na maofisa waliokuwa wanahudumu katika kitengo hicho watahamishiwa katika idara nyingine za Polisi.

Vilevile, taarifa ya Ofisi ya Rais Nigeria imethibitisha kutoa maagizo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi kufutwa kitengo hicho.