Habari

Diego Maradona: Muasisi wa "Bao la Mkono" Aaga Dunia

Kauli maarufu ya goli la mkono ilitokana na goli alilofunga Maradona kwenye mechi ya kombe la dunia dhidi ya Uingereza ambalo lilikuwa ni la mkono lakini muamuzi wa mchezo huo hakuona

Mwanasoka mashuhuri duniani, Diego Armando Maradona amefariki dunia leo akiwa nyumbani kwake nchini Argentina kwa mshtuko wa moyo, ikiwa ni siku chache tangu afikishe umri wa miaka 60.

Wiki mbili zilizopita, Maradona alifanyiwa upasuaji wa kuondoa fundo la damu kwenye ubongo. 

Taarifa za kusikitisha kuhusu kifo chake, zilithibitishwa mapema leo na Wakili wake na kupelekea taarifa hizo kuenea kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.

Maradona, aliondoka Hospitali Novemba 11, 2020, zikiwa ni siku nane tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa dharura wa ubongo. Mpaka mauti yanamkuta alikuwa kocha wa timu ya Gimnasia y Esgrima ya Argentina. 

Maradona anatajwa kama moja ya wanasoka bora kuwahi kutokea duniani. 

Akiichezea Timu ya Taifa ya Argentina kwenye michuano ya kombe la dunia la mwaka 1986, Maradona aliisaidia timu yake kutinga fainali na kutwaa kombe hilo.

Kauli maarufu ya goli la mkono ilitokana na goli alilofunga Maradona kwenye fainali hiyo dhidi ya Uingereza ambalo lilikuwa ni la mkono lakini muamuzi wa mchezo huo hakuona.


Licha ya kubarikiwa kipaji maridhawa na kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wenye ndoto za kucheza soka tamu, maisha yake nje ya uwanja yaligubikwa na uraibu wa pombe na madawa ya kulevya.

Taarifa zinasema kuwa Maradona, baba wa watoto wanne, alianza matumizi ya kokaini miaka ya 1980 na kupelekea uraibu ambapo aliendelea na matumizi kwa takribani miongo miwili.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa mwaka 1991, Maradona alisimamishwa na Timu yake ya Napoli kucheza kwa muda wa miezi 15 baada ya kufanyiwa vipimo na kugundulika anatumia Dawa ya Kulevya aina ya Kokein (Cocaine).

Tangu astaafu kucheza soka mwaka 1997, Diego Maradona amelazwa mara nyingi hospitalini kwa maradhi yatokanayo na unene na uraibu wa dawa za kulevya.

Mnamo mwaka 2000, nguli huyo machachari wa mchezo wa kabumbu alikaribia kupoteza maisha baada ya kuzidisha matumizi ya dawa za kulevya aina ya kokeini (cocaine) ambayo yalisababisha moyo wake kupunguza mapigo. Pia mwaka 2005 alifanyiwa tena upasuaji wa kupunguza unene wa mwili.

Katika michuano ya kombe la dunia yaliyofanyika nchini Urusi mwaka 2018, Maradona alirekodiwa akidondoka kwenye chumba cha watu muhimu (VIP box) wakati wa mechi kati ya Argentina na Nigeria.

Hayati Maradona amewahi pia kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Argentina kwenye michuano ya Kombe la dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2010.