Habari

Davido Avunja Mkataba na Lil Frosh kutokana na Unyanyasaji Dhidi ya Wanawake

Ni baada ya picha zinazomwonesha mpenzi wa Lil Frosh akiwa amevimba uso baada ya kupigwa kusambaa mitandaoni

Ulishawahi kufikiria athari zinazoweza kujitokeza kama mtu atajihusisha na unyanyasaji dhidi ya wanawake?

Picha zilizosambaa mtandaoni siku ya Jumatatu zilimuonesha binti ajulikanaye kama Gift Cammille akiwa amevimba uso baada ya kupokea kipigo kutoka kwa mpenzi wake Lil Frosh, msanii aliyeyekodiwa mnamo mwezi Septemba 14 chini ya lebo ya Davido Music Award (DWD) inayomilikiwa na msanii huyo nchini Nigeria, Davido.

Hii leo, kupitia mitandao yake ya kijamii, mwanamuziki Davido ametangaza kuvunja mkataba na Lil Frosh kwa kile anachodai kuwa lebo yake haiungi mkono unyanyasaji dhidi ya wanawake, hivyo wameamua kuvunja mkataba na msanii huyo na sasa hatambuliki kama msanii chini ya lebo yake.


Kaka na meneja wake Gift Cammille, Michael aliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kuwa hawana muda toka Gift ameruhusiwa hospitali baada ya kipigo hicho kilichosababisha majeraha ya ndani na bado hawajapeleka mashtaka hayo polisi.

“Binti huyo amekuwa akihudhuria hospitali mara kwa mara tangu wiki tatu zilizopita kutokana na majeraha ya ndani aliyoyapata baada ya kipigo alichokipata tarehe 15 mwezi septemba kutoka kwa mpenzi wake,” alisema Michael.

Msanii huyo anadaiwa kuwa na tabia ya kurudi na kuomba msamaha baada ya kumpiga mpenzi wake. Michael alisambaza pia picha za dada huyo akiwa amevimba baada ya kupigwa na ‘screenshots’ zinazoonesha Lil Frosh akimuomba msamaha binti huyo baada ya kumpiga.

Gift amekuwa akifanya kazi kama ‘video vixen’ na meneja wake ameweka wazi kwamba mwajiriwa wake amekuwa akikosa kazi kutokana na majeraha aliyoyapata.

Mpaka sasa, Lil Frosh hajatoa tamko lolote kuhusiana na madai yanayomkabili. Unyanyasaji dhidi ya wanawake ni tatizo kubwa nchini Nigeria kama ilivyo katika mataifa mengi barani Afrika, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwanamke mmoja kati ya watatu nchini humo ni mhanga wa ukatili huo.