Duniani

China Yapeleka Wanajeshi 60,000 Kwenye Mpaka na India

Mahusiano kati ya mataifa hayo yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani yameingia dosari kubwa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na mgogoro wa eneo la mpaka

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema kuwa China imepeleka wanajeshi 60,000 mpakani na India, ikiashiria kuwa mgogoro unaofukuta kuhusu eneo la mpaka kati ya majirani hao wenye idadi kubwa ya watu duniani haujapungua makali.

 

Nchi hizo zimeingia kwenye mgogoro wa kijeshi kutokana na kugombea eneo lililopo kwenye safu ya milima ya Himalaya ambalo ni mpaka wenye urefu wa kilomita 3440. Kwa kipindi kirefu, mpaka wa India na China haukuwekewa alama mahsusi zinazotambua upande wa India na ule wa China.


 

Picha: BBC 

Mahusiano kati ya mataifa hayo yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani yameingia dosari kubwa katika miezi ya hivi karibuni huku chanzo kikuu kikitajwa kuwa hatua ya India kujenga barabara mpya inayopita eneo la juu ya milima kuelekea kwenye kambi yake ya kijeshi ambayo ilianzisha mgogoro na wanajeshi wa China na kupelekea vifo 20 vya wanajeshi wa India. Pamoja na kuwepo kwa taarifa za vifo vya wanajeshi 43 kwa upande wa China, taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi duniani halikutoa taarifa ya kuthibitisha au kukanusha.

 

Uwepo wa Maziwa, Mito na Barafu katika maeneo hayo una maana kuwa mpaka unaweza kupindapinda na kupelekea wanajeshi kukutana mara kwa mara na kusababisha mapigano.

 

Kwa muda mrefu, mwaka 2020 umekuwa na mgogoro mkubwa zaidi katika bonde la Galwan. Mataifa hayo mawili yalishawahi kupigana vita moja pekee mwaka 1962 ambapo India ilishindwa vibaya.

 

Nchi zote mbili zinaangazia eneo hilo la mpaka kama muhimu kimkakati ikiwa utatokea mgogoro mwingine wowote. Ikiwa maafikiano ya kusitisha mapigano hayatofikiwa, wachambuzi wanasema kuwa mgogoro huo utaleta athari kubwa katika ukanda huo, ikiwamo kwa mataifa ya Pakistan, Japan na Australia na kwa uchumi wa dunia.

 

Vyombo vya habari vya serikali vimeonesha picha za wanajeshi wakipanda ndege za abiria kutoka jimbo la Hubei kwenda katika eneo ambalo halikuwekwa wazi. Picha zote na Weibo 


Vilevile, endapo mgogoro huo wa kijeshi hautomalizwa, hatari kubwa zaidi itatokana na ukweli kuwa mataifa hayo majirani yote yana silaha za nyuklia. Wachambuzi wengi wanasema kuwa mazungumzo ndiyo njia pekee ya kumaliza mgogoro huo kwani nchi zote mbili zina mengi ya kupoteza zikiingia vitani, ikizingatiwa kuwa China ni Mshirika mkubwa zaidi wa Kibiashara wa India.


Miezi ya hivi karibuni, Serikali ya India ilipiga marufuku aplikesheni 150 za China ikiwamo aplikesheni maarufu ya TikTok, ikisema kuwa ni kwasababu za kiusalama.