Habari

Benki ya Maendeleo Afrika Yaipatia Tanzania Mkopo Kupambana na Corona

Kwa Afrika Mashariki, Tanzania pekee ndiyo ilikuwa imebaki kunufaika na fungu hilo kutoka AfDB

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeidhinisha mkopo wa bilioni 117.57 ($50.7m) kwa Tanzania kwa ajili ya kupambana na madhara yaliyosababishwa na mlipuko wa virusi vya Corona.

Mkopo huo uliotolewa na mfuko maalum wa Benki ya Maendeleo unaohusika na Corona (CRF), unalenga kuongezea katika kiasi cha bilioni 252.77 kilichotengwa na Serikali ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya Tanzania katika kupambana na athari zilizoletwa na Corona, mkakati unaoungwa mkono na wadau  wengine wa maendeleo nchini.

Mkakati huo unakusudia kujenga uchumi imara huku ukipambana kupunguza athari za kijamii, kiuchumi, na kiafya zilizoletwa na janga la hilo  haswa kwa wafanyabiashara wa ndani  na kaya zilizo katika mazingira magumu na mfumo wa afya nchini.

Janga la corona nchini Tanzania limeongeza shinikizo kwenye vituo vya afya, mifumo ya ulinzi wa jamii na limepunguza ukuaji wa uchumi uliowahi kuiweka nchi kuwa miongoni mwa vinara Afrika Mashariki  kwa zaidi ya asilimia  6.2 wastani wa miaka mitano iliyopita.

Kwa sasa, ukuaji unakadiriwa kupungua kwa makadirio ya asilimia 6.4 hadi 3.6 na 2.6 kabla ya janga hilo.

Akizungumzia operasheni hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Nnenna Nwabufo alisema kuwa mkopo huo ulikuwa sehemu ya fungu kubwa zaidi kutolewa kwa nchi ambazo ni wanachama wa benki hiyo ikiwemo Tanzania.

“Corona na mabadiliko ya hatua za kuikabili hazitabiriki. Athari za kati na za muda mrefu za janga hili  bado hazijaeleweka kikamilifu . Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika linaboresha ushirikiano wake na serikali mbalimbali pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kuboresha namna inavyofatilia usimamizi wa janga hilo” Nwabufo alisema.

Mnamo Machi 23, 2020, Benki ya Maendeleo ya Afrika ilitoa tamko kuwa imetenga kiasi cha shilingi trilioni 6.96 ($3 billion) iliyokusanywa kwa muda wa miaka mitatu ili kusaidia kupunguza athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na janga la Corona kwa wanachama wa benki hiyo.

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania pekee ndiyo ilikuwa imebaki kwani nchi kama Kenya, Uganda, Sudani kusini, Rwanda, Burundi zilikuwa tayari zimeshanufaika na fungu hilo kutoka Benki hiyo.