Teknolojia

Aplikesheni Mpya ya Malipo ya Kidigitali Yazinduliwa Tanzania

Aplikesheni hiyo inatajwa kuja kuziba ombwe la kutokuwepo kwa suluhisho moja la malipo ya kidigitali Tanzania

Kampuni ya huduma za kifedha ya kimataifa ya Mastercard na kampuni ya Kitanzania inayotoa huduma za malipo Selcom wametangaza uzinduzi wa programu tumishi mpya ya kufanya malipo nchini.

 

Programu hiyo imekuja kuziba ombwe la kutokuwepo kwa suluhisho moja kwa malipo yote ya wateja nchini Tanzania kwa kuwezesha watu kuweka kadi zao zote za malipo au kuunganisha akauti zao za benki kwa njia ya aplikesheni kwenye jukwaa moja la kidigitali.

 

Vilevile, inaruhusu wateja wake kuunganisha kadi yao ya Mastercard au Visa (iliyotolewa na benki yoyote) na akaunti zao za benki za njia ya simu na kuwezesha kulipa maduka, migahawa na biashara zaidi ya 40,000 kwa kutumia Mastercard QR. Pia, mteja ataweza kununua muda wa maongezi wa ndani na wa kimataifa, kulipa huduma ya ving’amuzi vya televisheni na kubaini ofa na matangazo kutoka kwa biashara na migahawa.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom, Sameer Hirji amesema kuwa pengo kubwa ambalo programu hiyo itaziba ni uwezo wa kuunganisha kadi zote katika jukwaa moja. ‘’Pengo ambalo aplikesheni ya Selcom Mastercard inaziba ni uwezo wa kuunganisha kadi mkopo na malipo au aina nyingine za kadi katika aplikesheni moja na kuwalipa wafanyabiashara wanaotumia Mastercard QR bure, hasa ikiwa benki yako haikuwezeshi kufanya hivyo’’, amesema

 

‘’Selcom inajulikana kwa mawazo ya kibunifu yanaoleta mageuzi ya kisekta na aplikesheni hii ni mojawapo ya huduma nyingine nyingi ambazo tutazindua katika miezi ijayo ili kufanya maisha ya watumiaji na wafanyabiashara kuwa bora na rahisi’’, ameongeza Hirji

 

Kwa upande wa wateja kufahamu uwepo wa ofa mbalimbali, Selcom wanaamini kuwa watumiaji wanaweza kuongeza matumizi yao ya malipo ya kidigitali kwa kutumia Mastercard QR. Selcom ndiyo mtoaji mkubwa zaidi wa huduma za kifedha na malipo anayefanya kazi nchini Tanzania, akiwapatia wateja wake Tanzania na kote Kusini mwa Jangwa la Sahara, zana kamili za malipo ya keelektroniki na huduma zinazozingatia uchakataji wa malipo kidigitali, kwa kadi na bila kadi.

 

Meneja wa Nchi za Afrika Mashariki kutoka Mastercatd, Bw. Adam Jones amesema kuwa “Mastercard imekuwa ikiongoza mabadiliko ya malipo ya kidigitali kwa miaka kadhaa nchini Tanzania. Kwa kushirikiana na Selcom kuhamasisha watumiaji kulipia bidhaa na huduma kwa kutumia programu mpya ya Selcom Mastercard, sio tu kwamba tunakuza ujumuishaji wa kidigitali na kifedha, lakini pia tunaunganisha wafanyabiashara kwa wigo mpana wa wateja ili kuongeza kiwango cha shughuli zao za mauzo’’,