Habari

Afrika Kusini Kuuziwa Chanjo ya COVID-19 kwa Bei Ghali Mara Mbili ya Nchi za Ulaya

Dozi ya Corona itaigharimu Afrika Kusini dola 5.25 kwa kila dozi, (sawa na Tsh. 12,180), wakati nchi za Umoja wa Ulaya zikinunua dozi hiyohiyo kwa Euro 1.78 (sawa na Tsh 5000)

Afrika Kusini inatarajiwa kununua dozi za chanjo ya virusi vya corona ya Oxford-AstraZeneca kwa bei mara mbili na nusu zaidi ya nchi nyingi za Ulaya.

Afrika Kusini ndiyo nchi iliyoathirika zaidi na maambukizi ya COVID-19 barani Afrika, inatarajiwa kupokea dozi milioni 1.5 za virusi vya corona mwishoni mwa mwezi huu na mwezi Februari.

Shirika la Habari la AFP lilimnukuu afisa wa ngazi ya juu wa afya nchini Afrika Kusini akisema kuwa dozi ya Corona itaigharimu nchi hiyo dola 5.25 kwa kila dozi, (sawa na Tsh. 12,180), wakati nchi za Umoja wa Ulaya zikinunua dozi hiyohiyo kwa Euro 1.78 (sawa na Tsh 5000), kwa mujibu wa taarifa iliyovujishwa mtandaoni na Waziri wa Ubelgiji mwezi uliopita.

Taarifa hizi zinatia wasiwasi kuhusu uwazi wa nchi tajiri kushirikiana na nchi maskini katika utoaji wa chanjo hii, hasa katika bei na idadi ya chanjo inayotakiwa kutolewa kwa nchi maskini.

Shirika la Afya duniani, WHO, lilitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea kwa hali hii, ikiyataka mataifa tajiri kutojilimbikizia chanjo ya corona baada ya chanjo inayokidhi mahitaji kugunduliwa.

Afrika Kusini imeagiza dozi zingine milioni 18.5 za chanjo ya AstraZeneca ambazo zinatarajiwa kufika nchini humo kufikia nusu ya kwanza ya mwaka 2021.