Habari

ACT-Wazalendo Kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni Usaliti kwa Wazanzibari na Wapigakura Wake?

Ado Shaibu, Katibu Mkuu asema kuporwa kingi hakuhalalishi kususia kidogo kilichopatikana na kuwa serikali ya Umoja wa Kitaifa si Hisani ya CCM bali ni takwa la Katiba ya Zanzibar

Chama Kikuu cha Upinzani katika Visiwa vya Zanzibar, ACT-Wazalendo kimekubali kuungana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) hatua iliyohitimisha wiki kadhaa za tetesi na makanusho ya hapa na pale kutoka kwa viongozi wa chama hicho.

Tarehe 3 Desemba, 2020 Chama cha ACT-Wazalendo walitoa Taarifa kwa Umma kuwa Kamati ya Chama hicho itakutana Jijini Dar es Salaam katika kikao maalumu cha kujadili hali ya siasa nchini. Baada ya Kamati hiyo kukutana Taarifa kwa Umma ilitolewa jioni kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Ado Shaibu atazungumza na Wanahabari Desemba 6, katika Ofisi ya Chama Magomeni.

Katibu Mkuu, Ado Shaibu akiongea na waandishi wa habari alisema Kamati kuu ya chama chetu imeazimia kwamba, wawakilishi wachache kwa maana ya Madiwani, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge ambao wametangazwa kushinda waruhusiwe kushiriki kwenye vyombo vyao vya uwakilishi ili waendeleze mapambano kwenye vyombo hivyo.

''Ni muhimu ieleweke kwamba, kamati kuu imefikia uamuzi huu sio kwamba tunaufurahia, kamati kuu ilikuwa kwenye njia panda ya kuchagua njia moja kati ya njia mbili. Ilikuwa ni kuchagua ama uamuzi mbaya, ama uamuzi mbaya zaidi. Haikuwa chagua baina ya uamuzi mzuri sana na uamuzi mbaya, hilo ni muhimu sana lieleweke. Kwa hiyo tumechagua njia mbayo tumeona ina nafuu'', amesema Shaibu.

''Pili, kamati kuu ya chama chetu kwa kuzingatia ibara ya 9 (3) ya Katiba ya Zanzibar imeridhia chama kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar na imeielekeza Kamati ya Uongozi ya chama chetu kupendekeza jina la mwanachama atayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na muhimu ieleweke katika kuhitimisha, kamati kuu ya chama chetu imefikia maamuzi haya baada ya kufanya tafakuri ya kina'', ameongeza.

Katibu Mkuu, Ado Shaibu akijibu swali kuhusu kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuhalalisha Uchaguzi Haramu alisema, Hapana. ''ACT Wazalendo kimechukua na kinaendelea kuchukua hatua mbalimbali za ndani na nje ya nchi kuupinga uchaguzi huu na matokeo yake. Chama kitaendelea kufanya hivyo, ikiwemo kupigania Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi nchini unakuwa huru na wa haki'', Ado amesisitiza.

Akijibu pia swali kuhusu ikiwa kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni hisani ya CCM amekanusha na kusema kuwa SUK ipo kikatiba. ''Hatupewi na CCM. Tumepewa na Katiba ya Zanzibar. Majimbo tuliyotangazwa kushinda (Pemba) tulishinda kweli. Hata hivyo, Kuporwa kingi hakuhalalishi kususia kidogo kilichopatikana. Ni muhimu ikumbukwe pia kuwa SUK ni zao letu. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Ndugu Maalim Seif Sharif kwa kushirikiana na Rais Mstaafu wa Zanzibar Ndugu Amani Abeid Karume ndiyo waliokuwa waasisi wa SUK kwa ajili ya kuleta muafaka na maelewano miongoni mwa Wazanzibari.

Pia akiulizwa swali kuhusu ikiwa kujiunga na SUK si kuwasaliti waliokamatwa, kuteswa na kuuwawa, Katibu Mkuu huyo amedai kuwa si kweli kuwa ni kuwasaliti, bali chama chake kitaendelea kutetea halo yao ndani na nje ya nchi.

''Hapana. Vitendo vilivyofanywa na Vikosi vya Zanzibar, Vikosi vya JMT (Polisi, Jeshi, Usalama wa Taifa) vya kuuwa, kutesa na kujeruhi watu tena baadhi yao wakiwa mikononi mwa vyombo husika ni vitendo vya kijinai. Jinai haifi. Tutaendelea kutetea haki yao ndani na nje ya nchi hadi haki ipatikane na waliotenda unyama wawajibishwe,'' amesisitiza.

Vilevile, Ado amesema kuwa chama chake kujiunga na SUK hakutofifisha kesi ya chama hicho katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa Kijinai. ''Kuhusu kujiunga na SUK kutafifisha kesi ya ICC, Hapana. Chama hakitaachana na kesi yake ICC. Kesi itaendelea hadi waliofanya unyama kwenye Uchaguzi Mkuu wawajibishwe'', ameng'aka.

 

Historia ya Uchaguzi Zanzibar

Uchaguzi wa kwanza Viswani Zanzibar ulifanyika mwaka 1957 ambao ulihusisha Vyama vya Afro- Shirazi na Zanzibar Nationalist Party. Kwa kuwa sheria ya uchaguzi ya wakati huo iliruhusu wagombea binafsi katika uchaguzi huo pia walishiriki wagombea binafsi. Katika moja ya taarifa za mwaka za utawala wa wakati huo, uchaguzi wa mwaka 1957 ulielezewa kuwa na utulivu mkubwa katika historia ya Zanzibar. Katika Uchaguzi wa mwaka 1957 ni wapiga kura 39,833 tu ndio walioandikishwa kupiga kura. Ulikuwa ni Uchaguzi wa kuchagua Wajumbe sita ambao waliungana na wengine sita wa kuteuliwa na kuunda Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar.

Baada ya hapo ulifuata Uchaguzi wa Mwaka 1961, 1963, 1985, 1990, 1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020 ambazo kwa kiasi kikubwa zilikumbwa na sintofahamu nyingi kutokana na mtazamo kuwa chama tawala cha CCM na kilichokuwa kikuu cha Upinzani, Civic United Front (CUF) na sasa ACT-Wazalendo vinatoshana nguvu na ni vigumu kubashiri mshindi katika nafasi mbalimbali.

Hata hivyo Uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2005 ulianza na makubaliano ya muafaka wa pili kati ya vyama vya CCM na CUF makubaliano ambayo yalipelekea kufanyika kwa marekebisho makubwa katika mfumo wa uchaguzi Zanzibar. Mabadiliko haya yalikuwa ni kubadilisha mfumo wa uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar yaliyowezesha wawakilishi wawili wawili wa vyama vya CCM na CUF kuwa ni miongoni mwa Wajumbe waliounda Tume. Uchaguzi huo ulipofanyika, Dkt. Amani Abeid Karume wa CCM alishinda kwa kura 239,832 sawa na asilimia 53.2 na chama chake kupata Viti 31 vya Baraza la Uwakilishi na Madiwani 83.

Aliyemfuata alikuwa Seif Sharif Hamad ambaye alipata kura 207,773 sawa na asilimia 46.1 na Viti 19 vya Uwakilishi na Madiwani 58.

 

Historia ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Baada ya Uchaguzi huu wa 2005 kulitokea sintofahamu kubwa ambapo mgombea wa Upinzani Maalim Seif alipinga ushindi wa Dkt. Karume na kupelekea mazungumzo ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya Maridhiano yaliyofikiwa kati ya Dkt. Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad Novemba 5 2009, ili kuondoa uhasama wa kisiasa uliokuwa umejengeka baina ya Wazanzibari.

Kufuatia maridhiano hayo, Abubakari Khamis Bakar Muwakilishi wa Jimbo la Mgogoni aliwasilisha katika Baraza la Wawakilishi hoja binafsi kulitaka Baraza hilo kufanya mabadiliko ya katiba yatakayoruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Hoja hiyo ilikubaliwa na kukatungwa Sheria ya Kura ya Maoni namba 6 ya 2010 ambayo imeipa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar dhamana ya kuendesha Kura ya Maoni.

Tarehe 11 Mei, 2010 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimuagiza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuendesha Kura ya Maoni ifikapo tarehe 31 Julai 2010 ili kupata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar kwa kusema “NDIO” au “HAPANA” juu ya kuwepo kwa Muundo Mpya wa Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 31 Oktoba 2010.

Katika kura hizo za maoni walijitokeza wapiga kura 293,039 ambao ni sawa na asilimia 71.9 ya waliojiandikisha 407,669.

Waliounga mkono maridhiano na uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kupiga kura ya NDIO walikuwa 188,705 ambao ni asilimia 66.4 na waliopiga kura ya HAPANA ni 95,613 ambao ni sawa na asilimia 33.6.

Baada ya Uchaguzi ambao, Dkt. Shein alitangazwa mshindi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kura 179,809 sawa na asilimia 50.1 huku Maalim Seif wa CUF akipata kura 176,338 sawa na asilimia 49.1 na kupelekea kwa mara ya kwanza kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Uchaguzi wa 2015

Baada ya hapo ulifuata uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 ambao matokeo yalifutwa kwa mujibu wa Taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha iliyotolewa kupitia vyombo vya Habari siku ya tarehe 28 Oktoba, 2015.

Hatua hiyo ilipelekea ZEC, tarehe 22 Januari, 2016 kupitia vyombo vya habari kutangaza kwamba tarehe 20 Machi, 2016 kuwa ni siku nyingine ya kufanyika Uchaguzi wa marudio ambapo CUF na baadhi ya vyama vingine havikukubaliana na uamuzi wa Tume wa kufuta Uchaguzi na viliwaagiza Wagombea wote kuiandikia Tume barua ya kuyaondoa majina yao katika karatasi za kura.

Katika uchaguzi huo wa marudio vyama 14 vilishiriki na Dkt. Shein wa CCM aliibuka mshindi kwa kupata kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.

Hatua hiyo ilipelekea CUF kususia Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuiacha CCM kuwa na karibia asilimia 100 ya viti katika Baraza la Uwakilishi.

 

Uchaguzi 2020

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2020, ambapo Maalim Seif aligombania kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu na Chama hicho kiliripoti kwamba taribani wafuasi wao 17 walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa na vyombo vya usalama. Hatua hii ilipekea kiongozi wa Chama hicho, Ndugu Zitto Zuberi Kabwe kuandika barua kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) akituhumu vitendo mbalimbali walivyofanyiwa wafuasi wao visiwani Zanzibar.

Katika Uchaguzi huo Mgombea wa chama tawala CCM Dkt. Hussein Mwinyi alitangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya Urais kwa asilimia 76.27% huku mpinzani wake Maalim Seif wa ACT-Wazalendo akiwa mshindi wa pili kwa asilimia 19.87%.

Akiapishwa kuwa Rais wa nane wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi alisema atayaheshimu maridhiano kama ilivyo kwenye Katiba ya Zanzibar na yuko tayari kufanya kazi na Upinzani. Alisema ni wakati wa kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kufanya kazi kwa pamoja kuijenga Zanzibar.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar mshindi wa uchaguzi mkuu analazimika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na chama cha pili kwenye matokeo ili mradi kiwe kimepata asilimia 10 ya kura zote.

Alipoanza kuunda Serikali yake, Rais Dkt. Hussein Mwinyi alimteua Hemed Suleiman Abdalla kuwa Makamu wa Pili wa Rais na kuacha nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wazi na pia nafasi mbili za Uwaziri wazi ambazo zinatarajiwa zitachukuliwa na ACT-Wazalendo huku ikitarajiwa Maalim Seif atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kwenye gazeti la The Citizen la Novemba 20, 2020 Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif akihojiwa kuhusu uwezekano wa kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa alithibitisha kama chama wameshapokea barua ya kukaribishwa kwenye Baraza la Mawaziri lakini bado hawajaamua, bado wanaendelea na mashauriano. Lakini kutokana na kauli za viongozi mbalimbali wa Chama cha ACT-Wazalendo dalili zilikuwa zinaonyesha kwamba ni suala la muda tu Chama hicho kitakubali kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Novemba mwaka huu akifanyiwa mahojiano na wanahabari kwenye mtandao wa Zoom Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema, suala hilo linajadiliwa katika ziara ya mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad kutembelea waathirika wa matukio ya uchaguzi, akaongeza kama chama tuna michakato ya kidemokrasia, taarifa rasmi ya chama hicho haijatolewa na itatolewa baada ya vikao kukaa na kufanya maamuzi.

Zitto aliongeza, "Zanzibar ina historia ya kugombea uchaguzi na kukubaliana,” alisema.

“Tunakumbuka mwaka 1999 kulikuwa na mwafaka uliosimamiwa na Emeka Anyaoku aliyekuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola.”

Alitaja pia mwafaka wa pili wa mwaka 2001 na mazungumzo ya mwaka 2009 kati ya Rais Amani Karume ulioanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Kwa hiyo kuna mifano ya makubaliano, iwe ni kwa mwafaka au makubaliano. Tumewaambia wanachama wetu kwamba tunafanya vikao vya ndani. Kwa sasa siwezi kusema tutashiriki au hatutashiriki. Kwa sababu hiyo inategemea michakato ndani ya chama,” alisema.

 

Upinzani Mkali ACT-Wazalendo kujiunga SUK

Hatua ya Chama cha ACT-Wazalendo kukubali kuungana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) imekutana na Upinzani mkali kwenye mitandao ya kijamii ambapo watu mbalimbali wameona kama ni kusaliti harakati na misimamo waliyokuwa wanaisimamia hapo awali.

Baadhi ya watu maarufu mitandaoni kama Wakili Fatma Karume ambaye baba yake akiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume, alikuwa mmoja waasisi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kati yake na Maalim Seif mwaka 2009, amepinga vikali hatua hiyo akisema, "Mwanzo wa mwisho wa ACT. Someni historia ya MDC ya Zimbabwe na Tsvangirai. Maalim anaaga miaka 5 ya mwisho hii.

Swali: Nani ataweza kuhamasisha umma 2025? Bora mngeanza kuko-mpromise kabisa na Hussein leo ili Mkurugenzi akugaieni firgisi au shingo 2025, paja na kifua ndio basi."

Fatma aliongeza, "Kama bado hamjanielewa ni hivi; Maridhiano ya 2010 yalikuja ili kutuliza HAKI ya Kisiasa na kutengeneza Level Playing Field kwa vyama vya siasa. Katiba ikabadilishwa. Lakini bado kuna hitilafu kwenye Tume na Mahakama Huru ndio sababu ya matatizo ya 2015 na 2020"

Fatma aliendelea, "Maridhiano ya 2020, ACT wamepata nini? Maridhiano yana mantiki pale mnapobadilisha mfumo ili msikutane tena na tatizo lililoleta machafuko. 2025 ACT mtakutana na tatizo hili hili. You have kicked the can down the road but solved nothing. ACT have just legitimized the illegitimate"

Watu wengi wameonekana kutofurahishwa na hatua hiyo ya ACT-Wazalendo wakionyesha au wakilalamika kama ni usaliti kwa chama hicho kutokana na misimamo yake kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi kwa sababu wafuasi wao wengi waliumizwa kwa kukitetea chama hicho na sasahivi ni kama kinaungana na adui bila malalamiko yao kufanyiwa kazi.

Katika harakati za kampeni za uchaguzi, miongoni mwa masuala yaliyokuwa yakipigiwa kelele na ACT Wazalendo ni Masheikh wa Uamsho kushikiliwa katika magereza nchini bila kufunguliwa mashtaka au kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi. Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamehusisha tukio la kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama usaliti wa ACT-Wazalendo kwa Masheikh hao.

Wakati haya yakitokea, aliyekuwa Mgombea Urais wa ACT-Wazalendo ambaye ni mwanachama mwenye kadi namba 2 na Mshauri Mkuu wa chama hicho, Benard Membe ametangaza kuwa atajiondoa katika chama hicho rasmi tarehe 1 Januari 2021.

Membe alijiunga na Chama hicho Julai 16, 2020 na katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 aliibuka na kura 81,129 sawa na asilimia 0.5 ya kura zote. Bwana Membe Februari 28, 2020 alifukuzwa uanachama wa CCM na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Hatua ya ACT-Wazalendo kukubali kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inakuja wiki chache zikiwa zimepita tangu Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania Bara, CHADEMA kikiwa kimewatimua Wanachama wake waandamizi 19 kwa kukubali nafasi za Viti Maalumu na kwenda kuapishwa kinyume na msimamo wa chama.

CHADEMA kikiongozwa na Mgombea wake wa Urais kwenye uchaguzi wa Oktoba 2020, Tundu Lissu kinaendelea na msimamo wake wa kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu kuwa uligubikwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na haukuwa huru.